Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, usiku wa kuamkia leo katika hotuba ya televisheni kwa taifa tukufu la Iran, akisisitiza juu ya ulazima wa kuimarisha na kuendeleza kwa nguvu harakati ya Basiji katika vizazi vinavyofuatana kama "hazina kubwa, mwamko wa kitaifa na chombo cha kuongeza nguvu ya taifa," aliashiria kushindwa kwa Marekani na utawala wa Kizayuni katika kutekeleza malengo yao ya mashambulizi dhidi ya Iran kuwa ni dalili ya kushindwa kwa hakika kwao. Aidha, kwa kutoa nasaha kadhaa kwa taifa, aliwataka wananchi wote na makundi ya kisiasa kudumisha na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Akiashiria wajibu wa viongozi katika kuenzi Basiji, alisema Basiji ni harakati ya thamani ya kitaifa yenye motisha za kimungu na za dhamiri, yenye kujiamini na kujitolea. Akaongeza: kizazi cha nne cha Basiji, yaani vijana wadogo wapendwa kote nchini, kiko tayari kufanya kazi kwa juhudi. Harakati hii yenye thamani na muhimu sana ya Basiji inapaswa kukua, kuendelea, kukamilika na kuwa imara zaidi vizazi baada ya vizazi nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi alibainisha kuwa; uwepo wa harakati kama Basiji ni suluhisho na manufaa kwa kila taifa, na akaongeza: Taifa kama Iran ambalo limesimama waziwazi dhidi ya mababe na wahuni wa kimataifa na kujitokeza kifua mbele, linahitaji Basiji zaidi kuliko mataifa mengine yote.
Ayatollah Khamenei akisisitiza juu ya ulazima wa kujihami mataifa dhidi ya tamaa na kuingilia watawala wa mabavu, alisema: Kipengele kikubwa cha muqawama kilichoasisiwa na kukua nchini Iran leo kinaonekana katika kauli mbiu za kuinga mkono Palestina na Ghaza katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo nchi za Magharibi na hata Marekani. Alisema uhai na hari ya Basiji ni chanzo cha kukua kwa muqawama wa mataifa dhidi ya madhalimu wa dunia na akaongeza: Wanyonge duniani kutokana na kukua kwa muqawama wanapata hisia za kuungwa mkono na nguvu.
Kiongozi wa Mapinduzi katika kubainisha hakika ya Basiji alisema: Basiji katika sura yake ya kimuundo na kama sehemu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, mbele ya maadui ina sura thabiti na kwa wananchi ina sura ya kuhudumia. Lakini muhimu zaidi ni ngome pana ya Basiji ambayo imeenea kote nchini na ipo katika kila mtu na kikundi cha mashujaa, tayari kufanya kazi, chenye hamasa na matumaini, ikijidhihirisha katika nyanja za kiuchumi, viwanda, sayansi, vyuo vikuu, hawza, uzalishaji, mazingira ya biashara na nyanja nyinginezo.
Ayatollah Khamenei alieleza kuwa; “Basiji kwa ufafanuzi huu mpana na wa kijumla” ni chombo cha kufuta njama za adui katika nyanja za kijeshi, kiuchumi, uzalishaji, teknolojia na nyanja zote. Akasema: Wanazuoni wapendwa waliouawa kishahidi katika vita vya siku 12, wabunifu, watengenezaji na wapiga makombora, kila mtu aliyefafanua kwa hoja thabiti na kauli fasaha dhidi ya uvumi na vishawishi, madaktari na wauguzi waliojitoa muhanga ambao hawakuacha hospitali wakati wa vita, na mashujaa wa michezo waliodhihirisha mapenzi kwa Mungu, dini, nchi na taifa katika medani za kimataifa—iwe ni wanachama wa Basiji au la—wote hao ni Basiji. Aliongeza kusema: Imam ambaye alijivunia kuwa Basiji alikuwa akitafuta Basiji wa aina hii pana, Basiji isiyo ya tabaka maalum bali inajumuisha makabila yote, tabaka zote na makundi yote ya kijamii.
Kiongozi wa Mapinduzi katika nukta ya mwisho kuhusu Basiji aliwasisitizia viongozi wote wa taasisi za serikali kwa kusema: Fanyeni majukumu yenu kwa imani, hamasa na ujasiri, kama Basiji.
Ayatollah Khamenei katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuhusiana na masuala ya eneo na vita vya siku 12 alisema: Katika vita vya siku 12, taifa la Iran bila shaka liliwashinda Marekani na utawala wa Kizayuni. Walikuja na kufanya uovu lakini walipigwa na kurudi mikono mitupu bila kufanikisha malengo yao yoyote, jambo ambalo liliakisi uhalisia wa kushindwa kwao.
Akiashiria kauli kuhusu mpango wa miaka 20 wa utawala wa Kizayuni kwa vita dhidi ya Iran, alisema: Walipanga vita ambavyo ndani yake wangeweza kuchochea wananchi na kuwalazimisha kupigana dhidi ya mfumo wa Kiislamu, lakini mambo yaligeuka kinyume na walishindwa kiasi kwamba hata wale waliokuwa na mitazamo tofauti na mfumo walijiunga na mfumo, na mshikamano wa kitaifa ulijitokeza nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi alisema: Bila shaka nasi pia tulipata hasara na kwa mujibu wa asili ya vita, roho tukufu zilipotea, lakini Jamhuri ya Kiislamu ilionyesha kuwa ni kitovu cha azma na nguvu na inaweza kusimama kwa ujasiri bila kuogopa makelele, na kufanya maamuzi kwa nguvu. Aidha, hasara za mali walizopata maadui waliovamia zilikuwa kubwa zaidi kuliko hasara za mali zilizotupata sisi.
Alibainisha pia hasara kubwa za Marekani katika vita vya siku 12 na akaongeza: Marekani katika vita hivi ilipata hasara kubwa sana kwa sababu licha ya kutumia silaha za kisasa za kushambulia na kujihami, haikuweza kufanikisha lengo lake la kuwadanganya wananchi na kuwashirikisha nao, bali mshikamano wa taifa uliongezeka na Marekani ikashindwa.
Ayatollah Khamenei akielezea fedheha na aibu kubwa ya utawala wa Kizayuni katika janga la Ghaza—ambalo alilitaja kuwa moja ya majanga makubwa zaidi katika historia ya eneo—alisema: Marekani katika tukio hili iliungana na utawala wa haramu na ikapata fedheha na aibu kubwa, kwa sababu watu duniani wanajua kuwa utawala wa Kizayuni bila Marekani haungeweza kusababisha majanga makubwa namna hii.
Alimtaja kiongozi wa serikali ya Kizayuni kuwa ndiye mtu mwenye kuchukiwa zaidi duniani kwa sasa, na utawala wa Kizayuni kuwa bendi na taasisi yenye kuchukiwa zaidi duniani, na akaongeza: kwa kuwa Marekani ipo upande wao, chuki dhidi ya Wazayuni imeenea pia kwa Marekani.
Kiongozi wa Mapinduzi alibainisha kuwa; kuingilia kwa Marekani katika maeneo mbalimbali duniani ni miongoni mwa sababu za kuongeza kutengwa kwake, na akasema: kuingilia kwa Marekani katika kila eneo kunaleta uchochezi wa vita, mauaji ya kimbari, uharibifu na uhamishaji wa watu.
Alitaja vita vya Ukraine vilivyo na hasara kubwa na visivyo na matokeo kuwa mfano wa kuingilia Marekani, na akaongeza: Rais wa sasa wa Marekani aliyesema kuwa vita hivi angevimaliza ndani ya siku tatu, sasa baada ya takribani mwaka mmoja, yuko katika hatua ya kulazimisha mpango wa vipengele 28 kwa nchi ambayo wao wenyewe waliingiza vitani.
Ayatollah Khamenei alitaja mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, uvamizi wa Syria, jinai zake katika Ukingo wa Magharibi na hali mbaya ya Ghaza kuwa ni mifano mingine ya msaada wa wazi wa Marekani kwa vita na jinai za utawala huo mchafu. Akasema: Bila shaka kuna uvumi unaotengenezwa kwamba serikali ya Iran kupitia nchi fulani imetuma ujumbe kwa Marekani, jambo ambalo ni uongo mtupu na halijawahi kuwepo.
Akiashiria usaliti wa Marekani hata kwa marafiki wake kwa ajili ya kuwaunga mkono Mazayuni na jinai zake, na juhudi za kuchochea vita duniani kwa sababu ya mafuta na rasilimali za ardhini—ambazo leo zimeenea hadi Amerika ya Kusini—alisema: Serikali kama hiyo hakika si serikali ambayo Jamhuri ya Kiislamu inataka kushirikiana au kufungamana nayo.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatollah Khamenei alitoa nasaha kadhaa kwa taifa:
• Kwanza, kulinda na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Alisema: Tofauti kati ya tabaka na makundi ya kisiasa zipo, lakini muhimu ni kwamba mbele ya adui, kama katika vita vya siku 12, tuwe pamoja. Mshikamano huu ni kipengele muhimu sana kwa nguvu ya taifa.
• Pili, aliwasihi wananchi kumuunga mkono Rais na serikali. Alisema: Kazi ya kuendesha nchi ni ngumu na nzito, na serikali imeanza kazi nzuri ikiwemo kuendeleza miradi isiyokamilika ya shahidi Raisi, ambayo matokeo yake wananchi watayaona kwa idhini ya Mungu.
• Tatu, kuepuka matumizi mabaya katika mambo yote ikiwemo mkate, gesi, petroli na bidhaa za chakula. Alisema: Israf (matumizi kupita kiasi) ni miongoni mwa hatari na hasara kubwa kwa familia na taifa, na kama israf hii haitakuwepo, bila shaka hali ya nchi itakuwa bora zaidi.
• Mwisho, aliwasihi wananchi kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu, kunyenyekea na kuomba dua katika kila jambo ikiwemo mvua, usalama na afya, ili Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake aandae njia ya kurekebisha mambo.
Maoni yako